Hadithi za kweli

Hadithi ya JumaHadithi ya Stella

Mzee Banzi Kijiwe hujipatia pesa kwa kumlazimisha Juma Kombora Kambi kuomba omba mitaani. Wakati mwingine Juma hugoma kuomba mitaani na humwambia Mzee Banzi kuwa anataka kwenda nyumbani kwao Morogoro. Mzee Banzi humpiga sana Juma anapokataa. Juma Kombora ana umri wa miaka kumi tu kwahiyo hushindwa kijijitetea na pia ni mgeni katika mji wa Zanzibar. Maisha ya Juma ni ya kusikitisha sana na ni mara nyingi hulala na njaa kwa kuwa Mzee Banzi humwachia senti chache sana. Juma pamoja na vijana wengine wawili hulala mtaani chini ya usimamizi wa Mzee Banzi. Vijana hawa aliwaleta Mzee Banzi Zanzibar kutoka Morogoro kwa njia ya kuwalaghai wazazi wao.

Juma kabla ya kuja Zanzibar alikua anaishi Morogoro na mara nyingi alikua anatumia muda mwingi kuchunga mifugo ya baba yake Mzee Kombora Kambi na kucheza mpira wa miguu katika nafasi ya ushambuliaji. Juma alikua anapenda akiwa mkubwa kuwa mchezaji hodari mwenye uwezo mkubwa wa kupiga changa za maudhi kama Ronald. Lakini siku moja ghafla aliitwa na baba yake na kuambiwa kuwa ataenda Zanzibar na rafiki ya baba yake Mzee Banzi. Mama Juma alifurahi sana siku ya kumuaga Juma maana rafiki wa mume wake, Mzee Banzi, alimpa zawadi mama Juma ya kilo 25 za maharagwe na kilo 25 za mchele pamoja na vitenge doti mbili.

Mzee Banzi na Juma waliondoka Morogoro kwa basi mpaka mjini Dar es Salaam halafu wakapanda boti ya kasi mpaka njini Zanzibar. Juma alikuwa hajawahi kupanda boti maishani mwake kwahiyo alifurahi sana kupata nafasi hiyo.

Wazazi wa Juma wanamwamini sana Mzee Banzi na walitegemea atamsaidia Juma kupata kazi nzuri kwenye hoteli za kitalii mjini Zanzibar.

Juma hajuwi wapi atapata msaada na amebakiwa na ndoto tu za kuwa huru.

Stella Hiari Mwandunje mwenye umri wa miaka 16 aliletwa Dar es Salaam na shangazi yake Decorata Saini Makavu  kutoka katika kijiji cha Mawande,mkoani  Iringa.

Stella ni mtoto wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto saba. Wazazi wa Stella hawana kipato cha kutosha kuhudumia familia nzima. Baba yake Stella, mzee Hiari Mwandunje ni mzee mashuhuri sana kijijini Mawende.

Shangazi yake Stella aitwaye Decorata Saini alihamia Dar-es-Salaam kutoka Mawande kwenye miaka ya themanini mwanzoni. Tangu Shangazi Decorata alipohamia mjini amekua akitembelea kijijini kwao Mawande mara kwa mara. Kila wakati shangazi Decorata  alipokua anakuja kijijini huleta zawadi nyingi kutoka mjini pamoja na vitu vingi vya kisasa ambavyo  ni shida sana kupatikana kijijini. Kila mtu kijijini aliona kuwa maisha ya shangazi Decorata yamebadilika sana toka ahamie mjini na kuwa bora zaidi kutokana na vitu na misaada aliyokuwa anawapa wazazi wake kijijini. 
Mwaka 2006 mnamo mwezi wa kumi na mbili, shangazi Decorata alitembelea kijijini kwao Mawande kwa ajili ya kusherehekea sikukuu za krismas pamoja na wazazi wake kama ilivyo kawaida yake kila mwaka. Na kama kawaida yake alikwenda kutembelea familia ya mzee Hiari Mwandunje, baba yake Stella. Shangazi Decorata alimwelezea mzee Hiari masikitiko yake juu ya hali ngumu ya maisha ambayo inamkabili Mzee Hiari na familia yake. Shangazi Decorata alimwambia mzee Hiari kwamba angependa kujitolea kumsaidia mtoto mmoja wa kike, Stella. Mama yake Stella Bibi Genita Paskari hakuelewa kwanini shangazi Decorata amemchagua Stella wakati kulikua na wadogo zake ambao wangefaidika kielimu maana Stella alikua anasaidia kazi za nyumbani. Stella alikua anatambulika sana kwa kipaji cha kuimba kijijini mwao. Mama Stella alihisi kuwa hiyo inaweza kuwa ndio sababu kubwa ya kuchaguliwa mwanae Stella. Mzee Hiari  hupenda sana kumsifia mwanawe Stella kwa marafiki zake wakati akiwa anakunywa ulanzi, hupenda kusema, “mtoto wangu Stella ana sauti nyororo ya kumtoa nyoka pangoni”. Wazazi wa Stella walikubali kwa shingo upande kumtoa Stella maana walikua wanampenda sana mtoto wao.

Stella kwasasa anaishi kwenye nyumba ya Shangazi yake mjini Dar es Salaam. Shangazi yake aliwaahidi wazazi wa Stella kwamba akifika mjini, Stella atapata kazi inayomlipa vizuri na nafasi ya kwenda shule. Ndugu wengine wa familia ya Stella wanaishi Dar, kwahiyo Stella alijua kuna watu wakuwategemea wakati wa shida akifika Dar.

Stella hakujua jinsi jiji la Dar lilivyo kubwa na alipofika Dar aligundua kuwa ni vigumu kutembea mwenyewe  na hata kwenda kuwatafuta ndugu zake ambao wako Dar. Shangazi yake Stella, Decorata nae alivunja ahadi yake: Stella haruhusiwi kwenda shule na amefanywa kuwa mtumishi wa ndani kwa shangazi yake bila malipo. Stella hufanyishwa kazi masaa mengi na kama akikataa hupigwa na kutishiwa kufukuzwa  nyumbani kwa shangazi yake na kuachwa akajitegemee mitaani.Stella anatamani sana kurudi kwenye familia yake Iringa na pia kuwa na nafasi ya kwenda shule, lakini hawezi.

 
 
 

Kama unataka kupata habari au taharifa zaidi ya jinsi ya kuwasaidia wahanga wa usafirishaji na biashara haramu ya watu tafadhari wasiliana na

 
Child in the sun,
P.O. Box: 70509,
Dar es Salaam,
Tanzania
Tel: +255-0732924000, 0784 772155 / 0713321506
 
ZAYEDESA,
Mazizini Area,
Plot No.54,
P.O. Box 2331
Zanzibar,
Phone +255 24 2238520
Email: zayedesa@zanznet.com
 
Kiota Women Health and Development Organization
P.O.Box 10127 ,
Buguruni Malapa,
KIWOHEDE HOUSE NO 88
Phone : 255- 22- 2861111
Fax : 255- 22- 2861111
email :katri @africaonline.co.tz